Na
Mwandishi Wetu, Addis Ababa
MTANDAO wa jarida
mashuhuri duniani, the Econimist, wiki hii unmeibua mjadala mkubwa hasa Barani
Afrika baada ya kuchapisha makala inayomzungumzia Rais John Pombe Magufuli wa
Tanzania ikiponda staili ya utawala wake.
Katika makala hiyo
yenye anuani isemayo: “Tanzania’s new
president looks good but governs impulsively.” Makala hiyo inataka kujenga
dhana kuwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli anaonekana ameanza vyema ila utawala
wake unaongozwa na matukio!
Ukiisoma makala hiyo
ambayo kwa bahati mbaya au kwa sababu maalum haina hata jina la mwandishi (by-line)
utabaini mambo makubwa mawili: kwanza haina utafiti, inaonekana wazi kuwa
mwandishi alikurupuka tu akiwa na ajenda yake maalum kichwani.
Pili, utabaini kuwa
mwandishi ama anaowatumikia ni majeruhi wa mageuzi makubwa anayoendelea
kuyaleta Rais Magufuli na kwa hiyo anawasaidia jamaa zake kulialia au anatumiwa
na waliokuwa wakifaidika na mifumo dhaifu iliyokuwa awali. Nitaonesha punde kwa
nini naamini hivyo.
Nimelazimika kuwa na
mtazamo kuwa mwandishi anatumikia pande zote hizo mbili hapo juu si kwa sababu
napinga kukosolewa kwa Rais Magufuli au nchi yangu adhimu ya Tanzania. Kwa mara
nyingine nasema la hasha.
Naamini Rais Magufuli
anahitaji mawazo ya kujenga zaidi na kumtia moyo zaidi kutekeleza ajenda yake
ya mageuzi kuliko hata kusifiwasifiwa. Lakini ni rai yangu kuwa pale ambapo
Rais na Tanzania vinakosolewa basi mkosoaji anapaswa awe amefanyia utafiti hoja
zake kuliko kubeba ajenda za “wanamaslahi.”
Ukitaka kuamini vijenzi
vyangu viwili vya hoja (premises) kuwa mwandishi wa makala hayo hakufanya
utafiti na pili anatumikia ajenda flani, fuatana nami katika kupitia baadhi ya hoja
zake kuu na tutahitimisha kwa maoni ya wapigania maendeleo kote Afrika
walivyoitathmini makala hii.
Walimu wa Kenya
Moja ya hoja
inayoonesha dhahiri mwandishi ni mtu wa mrengo gani ni pale anapomlaumu Rais
Magufuli kwa utawala wake kuendesha msako wa wageni wanaofanyakazi nchini bila
vibali.
Akifichua kilichomuuma
zaidi, mwandishi huyo wa “the Economist” anaonekana akiandika kulalamikia
kufukuzwa kwa wageni wasio na vibali akishadidia kwa kuandika “wakiwemo walimu
kutoka Kenya!”
Si Magufuli tu, na wala
mwandishi asitake kujenga dhana kuwa hatua zinazochukuliwa Tanzania zinakiuka
haki za binadamu, bali dunia nzima kwa sasa hakuna nchi ambayo unaweza kuingia
na kufanyakazi bila kufuata taratibu ikiwemo kuwa na kibali cha kazi.
Kama mwandishi
ameumizwa sana na kuondolewa kwa wageni hao “wakiwemo walimu kutoka Kenya” basi
awashauri waombe vibali au waende kwenye nchi nyingine yoyote ya Afrika au
duniani ambako wataingia na kuanza kufanyakazi bila utaratibu wala kufuata
sheria za nchi.
Biashara Bandarini
Mwandishi katika makala
yake hiyo anaonekana kudhihirisha maslahi mengine anayoyapigania kupitia mgongo
wa kulaumu utawala wa Rais Magufuli. Hapa amesomeka akilaumu mabadiliko
yaliyofanyika Bandarini na kudai eti mizigo mingi sasa inapitia Mombasa badala
ya Dar es Salaam.
Kama kuna kituko katika
makala hiyo basi ni hiki. Kupungua kwa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam
kumefafanuliwa sana, moja la hakika ni kwamba licha ya kupungua mizigo hiyo
kutokana na kubana mianya ya kupitisha mizigo hovyo hovyo, Tanzania inajivunia
mapato yake kupanda kupitia Bandari hiyo.
Sasa zinapofanyika
jitihada kama hizi za kubadili mifumo ya utendaji ili Bandari itoe huduma bora na
pia Serikali ipate mapato yake, lakini akatokea mtu akaumia kutokana na haya
huyu ni wa kumhurumia lakini anayepaswa kuambiwa usoni na mchana peupe kuwa
hatua hizi kamwe “hazitarudi nyuma wala kusalimu amri.”
Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuboreshwa Zaidi |
Ujenzi wa taasisi
Katika hoja ambazo zinaonesha mwandishi wa makala
hiyo pia hakuwa anaelewa anataka nini ni hii. Ametoa hoja kuwa Rais Magufuli
hahitajiki kujenga utawala madhubuti bali ajenge taasisi madhubuti.
Nakubaliana naye kwamba ili nchi ipige hatua
inahitajika kuwa na taasisi madhubuti. Lakini ni hoja dhaifu mno kutetea uwepo
wa taasisi madhubuti kwa upande mmoja na kisha kudharau umuhimu wa viongozi
makini na madhubuti.
Ni kwa sababu hii ndio maana namshangaa mwandishi
huyo anapoonekana kuumizwa na utawala makini na madhubuti wa Rais Magufuli
unaotaka mambo yaende, unaotaka utendaji usio wa kimazoea na inayotaka Tanzania
ielekee kujitegemea.
Lakini hata kama tukubaliane na hoja dhaifu ya
mwandishi kuwa kuna umuhimu wa kujenga taasisi imara, nachelea kusema,
mwandishi huyo huenda hajawahi kufika Tanzania na amehadithiwa tu yanayoendelea
nchini.
Miongoni mwa taasisi zinazojengwa upya ni Shirika la Reli Tanzania (TRL) na tayari usafiri wa kisasa umeanza. tion |
Kwa kifupi, tangu aingie madarakani, Rais Magufuli
kwa kauli thabiti za hadharani, vitendo vyake na kwa lugha ya mwili wake
amepigania na ameanza kuzijenga taasisi za kitaifa ziweze kutenda kazi
ipasavyo.
Amewang’oa watendaji
kadhaa na wa taasisi muhimu kama Bandari, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa, Shirika la Reli n.k. Amewafikisha kortini wabunge waandamizi,
amewaambia majaji mchana kweupe kuwa watimize majukumu yao la atawashukia. Sasa
akitokea mtu hayaoni haya yanayoweka tu misingi kabla ya mageuzi zaidi kuna
shida mahali.
Kufuata sheria
Wakati hoja kadhaa
zilizopita zinadhihirisha maslahi anayoyatumikia mwandishi, hoja hii
inadhihirisha ni jinsi gani mwandishi wa makala husika anafuata hisia na
ushabiki na si kutafiti na kutafuta vithibitisho.
Anaonekana kulaumu eti
Rais Magufuli anawafukuza watumishi wa umma kazi hadharani na bila kufuata
taratibu za kisheria. Huyu ni dhahiri kahadithiwa kuhusu hili na mwalimu wake
naye anatatizo la kuongozwa na hisia na si uhalisia.
Tumesisitiza hapa mara
kadhaa kwamba uwezo wa Rais kuwateua na kuwaondoa watumishi wa umma katika
nafasi zao ni wa kikatiba na kisheria. Kikatiba, ibara ya 36 inazungumzia uwezo
wake wa kuteua na kutengua.
Kisheria, Sheria ya
Utumishi wa Umma, 2002 vifungu vya 23 na 24 vinaainisha taratibu ambazo Rais
anaweza kuzitumia katika kuwaondoa kazini watumishi wa umma. Sasa mwandishi wa
jarida makini kama “the Economist” anapofuata mkumbo bila utafiti ni aibu ya
karne kwa taaluma adhimu na adimu kama ya uandishi wa habari.
Maoni ya Wasomaji
Ukitaka kujua kuwa
makala hii ni miongoni mwa kazi dhaifu sana za sanaa kuwahi kutokea soma maoni
ya wasomaji kutoka kote Afrika na duniani waliochangia mwishoni tu mwa makala
hiyo ya mtandaoni.
Wengi katika
waliochangia si mashabiki wa kisiasa wa Dkt. Magufuli, si wanachama wa chama
chake wala siasa zake na wapo ambao hawajawahi kufika katika nchi yake lakini
wote wanaamini Dkt. John Pombe Magufuli ni aina ya Rais ambaye Tanzania
inamhitaji, Afrika ilimsubiri sana na Dunia inaheshimu uwepo wake.
“Magufuli anafanya
mageuzi yenye mtikisiko katika uchumi wa Tanzania; akipambana kukusanya kodi,
kuzuia ufisadi na kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje…wengi wataumizwa na
mageuzi haya,” ameandika msomaji mmoja akijibu na kupingana na hoja dhaifu za makala
ya “the Economist.”
Mwingine akaandika: “Ni
wazi mwandishi hajui nini kinaendelea Barani Afrika. Hili ni Bara ambako
wafanyabiashara wengi wakubwa wamekuwa ni wezi wazuri. Haya, anaibuka Magufuli akiwa
analijua hilo na kuanza kubadili mambo, the Economist linasimama upande wa
wezi!”
Nihitimishe, kwa
kusisitiza tena, litakuwa ni wazo la kijinga kudhani kwamba Watanzania hawataki
Rais wao wala Serikali yao ikosolewe, la hasha. Mwalimu Nyerere ametuasa katika
“TUJISAHIHISHE” na “MWONGOZO WA TANU” kuwa kujikosoa ni kujisahihisha. Lakini
Abraham Lincoln alipata kusisitiza:
“He has a right to
criticize, who has a heart to help,” kwamba haki ya kukosoa anayo tu yule
mwenye nia ya kusaidia. Mwanafalsafa nguli wa kale Plato yeye anatuonesha kuwa
ukiona zinakuja kosoakosoa zisizo na msingi ujue kuwa kuna kitu kikubwa umefanya
na ukiona kimya ujue haujafanya lolote, anasema: “To avoid criticism, do
nothing, say nothing, be nothing.”
Alamsiki.
*Mwandishi
wa makala haya amejitambulisha kuwa ni Mtanzania aliyebobea katika masuala
mbalimbali ya maendeleo endelevu na makala haya yamechapishwa kwa mara ya
kwanza katika gazeti la Jamboleo la Jumapili Mei 29, 2016.
Comments
Post a Comment